Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mhe.Fideli Ndelego amehimiza Watendaji wa Kata na vijiji, Maafisa Elimu Kata pamoja na Walimu Wakuu wa Shule kwa kushirikiana na kamati za wazazi Shuleni wahakikishe Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wanapata chakula Shuleni.
Amesema hayo katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi Februari tarehe 02, 2023, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Baraza la Madiwani liliwashirikisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya, Kaimu katibu Tawala Wilaya ya kakonko, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa vyama vya Siasa, Wakuu wa Divisheni na Vitengo, Watendaji wa kata, Viongozi wa Dini pamoja na Wananchi.
“Wananchi wa Wilaya ya Kakanko wanatakiwa kuwa na utaratibu wakuwapatia Watoto chakula Shuleni na kuwapeleka Shuleni bila kusukumwa, hatutakuwa tayari kuona Mzazi anamkataza mtoto wake kupata chakula Shuleni”
Ameendelea kusema lengo la kuwepo kwa Baraza la Madiwani ni kuendeleza usitawi na maendeleo ya Wananchi wa Kakonko. Hivyo Madiwani wanaahidi kushirikiana, kushikamana na Wananchi ili kuleta mabadiliko na maendeleo chanya katika Wilaya ya Kakonko. Aidha baraza la Madiwani limewataka Wazazi wote ambao bado hawajawapeleka Watoto Shule kuhakikisha wanawapeleka pia viongozi waendele kuhamasiha jamii juu ya umuhimu wa Elimu kwa kuwapatia Watoto haki yao ya msingi ya Elimu.
Kwa upande wake Kanali Evance Mallasa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ameeleza kila Shule inatakiwa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi angalau mlo mmoja kwa siku, hivyo Wazazi/Walezi wanao wajibu wa kuchangia chakula Shuleni ili Watoto wapate huduma ya chakula. Amesisitiza kila Shule iwe na shamba darasa kwa ajili ya kulima mazao ya Chakula na kila mwanafunzi apande angalau mti mmoja wa matunda ili Watoto wawe na afya bora.
Alihitimisha kwa kusema jamii bado ina mwamko duni juu ya umuhimu wa Elimu kwani mpaka sasa katika zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza Wilaya ya Kakonko bado haijafikisha asilimia 100%. Hivyo Watendaji wa kata na vijiji, Maafisa Elimu Kata pamoja na Walimu wakuu wa Shule wahakikishe Watoto wote ambao wamefikia umri wa kuanza Shule waandikishwe.
“Sisi Viongozi tumepata fursa yakuweza kuelewa umuhimu wa Elimu tutumie nafasi hii kuweza kuwaelimisha na wenzetu”
Naye Afidhi Ramadhani Mtendaji wa Kata ya Katanga amesema kuwa kutokana na wazazi kutokuwa na uelewa juu ya umuhimu wa Elimu ndiyo sababu ya kutowapeleka Watoto wao Shule na badala yake kuwapeleka kwenda kufanya kazi za ndani, hivyo kama viongozi wanaowajibu wakuendelea kutoa Elimu kwa wazazi/walezi kwani wengi wao wamekuwa na dhana kwamba wengi waliosoma bado hawaja ajiliwa kupitia dhana hiyo wataendelea kuwa na nguvu kazi isiyokuwa na Elimu
Mkazi wa Wilaya ya Kakonko Naftali Kilaha amesema Wazazi wengi wamekuwa na dhana kwamba hawana uwezo wa kuwapeleka Watoto wao Shule na badala yake kuwashauri kufanya vibaya katika Masomo yao na kuwapeleka mjini kufanya kazi za ndani pia kuwashauri Watoto wa kike kwenda kuolewa jambo ambalo linasababisha matatizo kwa wazazi na jamii kwa ujumla.
Naye Afisa uchunguzi TAKUKURU Ndugu Nelson Kailembo Wilaya ya Kakonko ametumia fursa ya Mkutano wa Baraza la Madiwani kutambulisha Programu ya “TAKUKURU Rafiki” kuwa ni program iliyoanzishwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa lengo kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kuzuia rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa