Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa amewaasa wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii inayowazunguka na watoto kutoa taarifa mapema wanapofanyiwa ukatili.
Akiwakilishwa na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Kakonko ndugu Amani Alexander katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika katika uwanja wa shule ya msingi Maendeleo mwishoni mwa wiki tarehe 16 Juni, 2022 amebainisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni pamoja na ukatili wa kijinsia, kingono, kielimu, kisaikolojia na ndoa za utotoni.
“Ndugu zangu takwimu za kituo cha simu ya huduma ya mtoto zinaonyesha watoto wanapitia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vipigo kutoka kwa wazazi, walezi na walimu, kubakwa, kulawitiwa, mimba na ndoa za utotoni pia wanatumikishwa katika kazi zisizoendana na umri wao na hata kukosa haki zao za elimu”, alieleza ndugu Alexander Alex.
Akitoa historia ya chimbuko la kuwepo siku ya mtoto wa afrika, Anastazia Maulid mwanafunzi anayesoma katika shule ya msingi Kakonko na kufanya Sanaa katika kikundi cha vijana Kakonko (At youth Group Kakonko) ameeleza kuwa Watoto wa afrika waliandamana kudai haki zao mbele ya wazungu lakini Watoto hao waliuwawa na wazungu hao kikatili hivyo Watoto wana haki na wanatakiwa kupendwa na kuishi.
Diwani wa Kata ya Kakonko Mhe. Augustino Linze alieleza siku ya mtoto wa afrika ni ya wazazi kukumbushana namna ya kuwalea watoto kwani bila watoto kuwepo hakuna taifa.
Akitoa utekelezaji wa shughuli zakumlinda mtoto kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2022 afisa Maendeleo ya Jamii bwana Stephen Mabuga alieleza kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo zikiwemo taasisi binafsi na mashirika ya kimataifa wamekuwa wakifanya jitihada kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na ulinzi kwa mtoto unakuwepo shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya mtoto imetolewa kwa kata tatu ambazo ni Mugunzu, Kakonko na Kasanda ambapo shule za msingi 11 zimefikiwa na watu 6513 wamefikiwa.
Miongoni mwa Walioshiriki katika maadhimisho hayo ni Shirika la World Vision ambao ndio wadhamini, Mkurugenzi mtendaji, Wasaidizi wa Sheria (Washeka), Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya, Madiwani, Walimu, Viongozi wa dini Wanafunzi na wazazi.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Juni huku tukikumbuka matendo ya ukatili yaliyofanywa kwa Watoto huko Soweto nchini Afrika Kusini na mwaka 2022 Kauli mbiu inasema,
“Tuimalishe Ulinzi wa Mtoto, Tutokomeze Ukatili dhidi yake, Jiandae kuhesabiwa”.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa