Serikali Wilayani Kakonko imetoa muda wa siku saba kwa wazazi na walezi ambao hawajawapeleka wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza baada ya shule kufunguliwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa Katika kikao cha Baraza la Ushauri la Halmashauri (DCC) kilichofanyika Januari 09, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo Wilayani Kakonko. Katika kikao hicho amewaagiza Viongozi wa Kata, Vijiji na Walimu wakuu kuhakikisha wanashirikiana kuwabaini Wanafunzi ambao hawajaripoti Shuleni.
Maagizo hayo yametolewa baada ya wanafunzi 2934 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza Wilayani Kakonko hadi kufikia Januari 09, 2024 wanafunzi ambao wameripoti wilayani humo ni wanafunzi 341 sawa na asilimia 11.7 baada ya shule kufunguliwa huku idadi hiyo ikitajwa kuwa ndogo ikilinganishwa na wanafunzi walichaguliwa.
Aidha, amesema licha ya Serikali kukamilisha miundombinu muhimu katika shule za Msingi na Sekondari baadhi ya wazazi na wanafunzi wamekua na mwamko mdogo katika suala la elimu jambo ambalo linapelekea wanafunzi kuchelewa kuripoti shuleni.
Pia Kanali Mallasa ameendelea kusema kwa wazazi ambao watashidwa kuwapeleka watoto shuleni hatua za kisheria zitachukuliwa hivyo amewaagiza Watendaji wa kata waendelee kufanya ufuatiliaji wa kuwabaini wazazi/walezi ambao hawajawapeleka wanafunzi shuleni kwani kitendo hicho kinakwamisha jitihada za serikali katika suala la elimu.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndg. Michael Faraay, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu ya elimu ambayo imesaidia kutatua changamoto ya madarasa katika Shule za Msingi na Sekondari.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa