Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mhe.Fidel Nderego amewataka wazazi kuwapeleka watoto shuleni wakapate haki yao ya msingi ya elimu kwani Serikali itachukua hatua za kisheria kwa Wazazi watakaobainika kuwa na watoto watoro.
Mheshimiwa Nderego ameyasema hayo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la robo ya kwanza katika mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri siku ya Ijumaa tarehe 11 Novemba, 2022.
Akisisitiza kuhusu suala la utoro, Mwenyekiti wa Halmashauri aliwaagiza Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanafuatilia mahudhurio ya Wanafunzi Shuleni kwa kukagua daftari la Mahudhurio ili kila mmoja akawajibike kwa nafasi yake na kushiriki katika kukomesha suala la utoro kwa Wanafunzi.
Diwani wa kata ya Nyabibuye January Basililo alieleza kuwa ili watoto wapende shule inatakiwa kuwepo na vivutio kama viwanja vya michezo na vifaa hivyo kutaka kujua mpango wa Serikali kuhakikisha viwanja vya michezo vinajengwa ili kupunguza utoro shuleni.
Kaimu Afisa Elimu msingi Jacob Bada alitoa ufafanuzi kuwa katika fedha za uendeshaji wa shule (capitation) zinazoletwa katika shule kuna kipengele cha ununuzi wa vifaa vya michezo hivyo kuwasisitiza waalimu wakuu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kuboresha mazingira ya viwanja na kununua vifaa vya michezo shuleni.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa