Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kutoka katika kata 13 zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko wamejengewa uwezo kwa kupata mafunzo yatakayo wasaidia kujua majukumu na mipaka ya nafasi zao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa wananchi wao. Mafunzo hayo yamefanyika kwa mda wa siku mbili katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Wilayani Kakonko ambapo yametamatika leo Tarehe 13,Januari 2025.
Akifunga Mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa,amewataka wenyeviti hao kusimamia vizuri matumizi bora ya ardhi, ambapo ameeleza kuwa kumekuwepo na changamoto ya migogoro ya ardhi katika maeneo yao kwa hali hii imekuwa ikichangiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji ambao wamekuwa wakikosa uandilifu katika kutimiza majukumu yao. Hivyo ameendelea kuwasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha Col.Mallasa amewapongeza wenyeviti hao kwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa mitaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27 2024 na kueleza kuwa hana wasiwasi na viongozi hao waliochaguliwa kwani kama wilaya wataendelea kutoa ushirikiano kwa pamoja katika kutekeleza majukumu ili kuijenga Kakonko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndg Ndaki Stephano Muhuli, ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa lengo la kuwakumbusha na kuwaelekeza majukumu mbalimbali ya utendaji wa shughuli za kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo amewataka kwenda kusimamia fedha za serikali zinazokusanywa katika maeneo yao na kutoa taarifa fedha zinapoingia kwani katika vijiji vyao kuna vyanzo vingi vya ukusanyaji wa mapato. Ameendelea kuwasisitiza kuendelea kutatua kero za wananchi katika maeneo yao hivyo waendelee kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabiri wananchi.
Naye Bi.Sarah Kilagane, Mwezeshaji kutoka Chuo cha serikali za mitaa Hombolo, amezungumzia majukumu ya mwenyekiti wa kijiji ikiwemo kuwa mwenyekiti wa vikao vya kijiji, kuwakilisha wananchi katika kamati ya maendeleo ya kata na kutatua migogoro mbalimbali ya wananchi ambayo haina ulazima wa kufika katika mamlaka au ngazi nyingine.
Baadhi yao wameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi kwenda kutekeleza yale yote waliyoelekezwa kwenye mafunzo ikiwa nikuendelea kutatua changamoto za wananchi na kusimamia fedha za serikali pamoja na matumizi bora ya ardhi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa