Wawezeshaji wa Vituo vya MEMKWA wamehimizwa kufanya vizuri zoezi la uandikishaji wa watoto wasiosoma shule wenye umri wa miaka 09-15 ili kujiondoa katika mpango wa MEMKWA.
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi wa Mafunzo Ndugu Amani Alexander Kanguye Kaimu katibu Tawala (W) ya Kakonko wakati alipokaribishwa kufungua Mafunzo ya Wawezeshaji wa Vituo vya MEMKWA yatakayodumu siku tano (5) kuanzia Machi 20 -24, 2023, yanayofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
“Wilaya ya Kakonko tunatarajia iwe ni Wilaya ambayo itakua kinara kwa Mkoa wetu wa Kigoma na ikiwezekana Mkoa wa Kigoma uwe ndio kinara katika zoezi la uandikishaji wa watoto wasiosoma Shule wenye umri wa miaka 09-15 kwa mikoa mitatu iliyobainishwa ili kujiondoa katika takwimu za MEMKWA, Hivyo washiriki wazingatie wanayofundishwa ili kasi ya uandikishaji iongezeke, alieeleza Mgeni rasmi.
Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Dar es Salaam, Ndugu Chediel Mlavi ameeleza lengo la mradi wa MEMKWA ni kuongeza uandikishaji, kuondoa watoto ambao hawako Shuleni, kubuni mbinu zitakazowezesha darasa endelevu la MEMKWA kuwa endelevu, kufundisha Stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika pamoja na kuboresha Stadi za maisha kama ujasiliamali ili kuchangia maendeleo ya Jamii.
Aidha amesema Elimu ya MEMKWA yaani mpango wa Elimu kwa Watoto Walioikosa hutolewa kwa kundi rika la vijana wenye umri wa Miaka 14-18 na katika programu ya Elimisha Mtoto hutolewa kwa watoto wenye umri wa miaka 09-13 na baadae wanajiunga na mfumo rasmi wa Elimu kuanzia darasa la Nne na la Saba.
Hivyo wawezeshaji wa vituo vya MEMKWA wanatakiwa kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto waliokosa (MEMKWA).
Kwa upande wake Afisa Elimu Watu wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi Ndugu Majaliwa Tryphone amesema kasi ya uandikishaji wa watoto wasiosoma Shule bado ni ndogo hivyo wawezeshaji wahakikishe wanafikia malengo ndani ya muda uliopangwa kwa kufanya zoezi hilo vizuri kwani mpaka sasa watoto walioandikishwa ni 300 kati ya watoto 620 wanaotakiwa kuandikishwa ndani ya mwaka mmoja kwa vituo husika ndani ya Wilaya ya Kakonko.
Washiriki wa Mafunzo hayo ni Pamoja na na Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu na Walimu Wanaofundisha Vituo Vya MEMKWA na mafunzo yanafadhiliwa na Shirika la UNICEF.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa