Zoezi la utambuzi na uhamasishaji linalolenga kuandikisha na kuanza masomo nje ya mfumo rasmi kwa watoto kuanzia miaka 07-15 na wale ambao waliacha masomo limeanza siku ya alhamisi Januari 30, 2025 Wilayani Kakonko katika kata ya Kakonko.
Zoezi hilo limeanza kwa kutoa elimu kwa wazazi na walezi na kuwabaini watoto wasiopata elimu chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa mataifa (UNICEF) na kuongozwa na kamati ya Uhamasishaji ngazi ya kata ikihusisha Afisa elimu kata, diwani, mwenyekiti wa Kijiji, afisa mtendaji wa kata na kijiji pamoja na Wahudumu ngazi ya jamii.
Akizungumza katika zoezi hilo Afisa elimu watu wazima, Mwalimu Majaliwa Trayphone ameeleza kuwa zoezi hilo limeanza kwa ufanisi kwani wazazi wengi wamejitokeza hivyo amewaomba wazazi kutoa ushirikiano kwa kuwapeleka watoto kujiandikisha ili waweze kupata elimu.
Ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF watahakikisha watoto hao wanapata elimu na kupata vifaa vitakavyosaidia katika kuendelea na kuhudhuria vipindi vya masomo.
Aidha ameendelea kusema zoezi hilo litaendelea kufanyika kwa kuendelea kutoa elimu kwa wazazi, walezi na jamii kupitia mikutano ya hadhara,viongozi wa dini pamoja na matangazo mbalimbali.
Uandikishaji wa watoto wenye umri wa miaka 07-15 katika masomo ya MEMKWA unalenga kuwafikia Watoto ambao hawakuwahi kusoma, watoro, walioacha shule ili kujenga stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa lengo la kuwaingiza katika mfumo rasmi wa masomo hapo baadaye.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa