Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya magharibi, Jumanne Wagana amekabidhi madawati 50 leo Alhamisi Novemba 09, 2023 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuchangia katika miradi ya Jamii.
Akikabidhi madawati hayo, Meneja Wagana ameeleza kuwa ni utaratibu wa benki ya CRDB kutenga 1% ya faida wanayoipata kila mwaka kuifikia jamii katika maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa CRDB inaamini madawati hayo yataleta chachu na mabadiliko katika ufaulu wa wanafunzi ambao ni viongozi wa baadaye.
Mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi madawati, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amewashukuru Menejimenti ya benki ya CRDB kwa kuwapa heshima na kuwapa mchango wa madawati ambao unalenga kuboresha mazingira ya Elimu katika Wilaya ya Kakonko.
“Serikali bado ni muumini mkubwa wa Maendeleo shirikishi hivyo Serikali imekuwa ikahamasisha na kuhamasisha juu ya umuhimu wa Wananchi, Taasisi pamoja na wadau mbalimbali kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo nchini”, alieleza Kanali Mallasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndaki Stephano Mhuli aliishukuru benki ya CRDB mchango wa Madawati walioutoa na kusisitiza Uongozi wa Kata Kukaa na Wazazi ili kuboresha hali za watoto hususani Mavazi.
Halfa ya kukabidhi madawati 50 imefanyika katika shule ya msingi Ruyenzi iliyopo katika kata ya Kiziguzigu na kuhudhuriwa na Mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Elimu Msingi, Viongozi wa shule, Kijiji, Wazazi na wanafunzi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa