Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col.Evance Mallasa amezindua rasmi gari jipya la Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, aina ya Toyota Landcrusier 250 Prado (All Rounder) lenye thamani ya Tshs.252,384,800 katika ofisi za Halmashauri Jumatano Januari 22, 2025.
Akizindua gari hilo, Kanali Mallasa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watumishi wake kwani upatikanaji wa gari hili utasaidia kuleta tija na motisha kwa watumishi wengine na kuongeza chachu ya kufanya kazi kwa wakati.
Aidha Mkuu wa Wilaya amesisitiza gari hilo litunzwe vizuri kwa kufanyiwa matengenezo kwa wakati na kuzingatia utaratibu wa uendeshaji wa gari la viongozi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji, Ndaki Stephano Mhuli amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa gari hilo. Hata hivyo ameeleza kuwa gari hilo lilikuwa linunuliwe katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 lakini Menejimenti ilipendekeza kununua lori kama chanzo cha mapato ambapo hadi sasa mapato ya Halmashauri yamepanda kutokana na gari hilo.
Akitoa maelezo kuhusu mchakato wa manunuzi wa gari hilo, Afisa Mipango wa Wilaya, Michael Faraay ameeleza kuwa Serikali kuu ilitoa milioni 220 kwa ajili ya ununuzi wa gari la Mkurugenzi Mtendaji, Hata hivyo Halmashauri kupitia mapato ya ndani ilifanikiwa kuongeza milioni 32 ili kukidhi mahitaji halisi ya ununuzi wa gari hilo ambalo litasaidia shughuli za maendeleo na kuhudumia Wananchi kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa