Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Jimbo la Buyungu, Ndaki Stephano Mhuli amefanya kikao na wazee maarufu 19 kutoka kata 13 za Wilaya ya Kakonko kuwapitisha katika mambo muhimu ya uchaguzi na kuwasisitiza kuhamasisha jamii kujitokeza kujiandikisha tarehe 11-20 Oktoba, 2024 ili kupata uhalali wa kushiriki kupiga kura Novemba 27, 2024.
Akiongea na wazee hao leo Alhamisi Oktoba 3, 2024 katika ukumbi wa Gombe uliopo ofisi za Halmashauri Wilayani Kakonko amewaomba wazee hao kuendelea kuombea uchaguzi na kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kuwa na afya njema.
Aidha Msimamizi wa Uchaguzi amewasisitiza wazee maarufu kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na uvumilivu na staha bila kujali itikadi za kisiasa wakati wote wa Uchaguzi hususani wakati wa kampeni ili kuendeleza amani iliyopo kwani ndio kitu muhimu kwa nchi.
Mzee Juma Maganga aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwashirikisha wazee katika hatua za awali za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuiomba jamii hususani vijana kujitokeza kujiandikisha ili kuweza kushiriki kupiga kura na kuchagua Viongozi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.
Msimamizi wa Uchaguzi amekuwa akifanya hamasa na kutoa elimu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kukutana na makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na leo amekutana na Wazee maarufu.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa