Mafunzo kwa waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki yamefanyika Wilayani Kakonko leo Jumanne Aprili 29, 2025 huku washiriki wakila kiapo cha kutunza siri na kujitoa uanachama kabla ya kuanza zoezi la uboreshaji wa awamu ya pili kuanzia tarehe 1-7 Mei, 2025.
Akifungua Mafunzo hayo Afisa Mwandikishaji, Michael Faraay, ameeleza kuwa mafunzo hayo yatahusisha namna bora ya ujazaji wa fomu kwa kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya bayometriki.
Aidha ameeleza kuwa mawakala wa vyama vya siasa watakuwepo katika vituo vya kuandikishia wapiga kura kwa lengo la kuwatambua wapiga kura wa eneo husika na kupunguza vurugu zinazoweza kujitokeza katika kituo cha uandikishaji.
Hata hivyo, afisa mwandikishaji amefafanua kuwa mawakala wa vyama vya siasa hawatakiwi kuwaingilia majukumu yao waandikishaji wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wakiwa katika vituo vyao vya kazi.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha usalama ili zoezi liweze kufanyika kwa ufanisi hivyo amewataka washiriki kuwa na ushirikiano kwa watendaji wote wa uboreshaji wa daftari pamoja na watendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi pindi watakapokuwa na changamoto yoyote inayoweza kujitokeza katika vituo vyao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji, Ndaki Stephano Mhuli amewataka washiriki kufanya kazi kwa kujituma na kutanguliza uzalendo pamoja na kumshirikisha Mungu huku wakizingiatia maelekezo yote waliyopewa wakati wa mafunzo.
Mafunzo haya ya siku moja yamehusisha wasimamizi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki 72 ambapo 46 sawa na watumishi 02 kwa kila kituo wataanza kazi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kuanzia tarehe 1-7 Mei, 2025 na wengine 26 watakuwa waandishi wasaidizi wa akiba. Aidha mafunzo hayo yamehudhuriwa na wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata 13, wasimamizi wasaidizi ngazi ya Jimbo 8 na watendaji wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa