Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa amewahimiza Wananchi kutenga maeneo ya kupanda miti kama hifadhi ya misitu na kuitunza ili kuwa chanzo cha mapato kwa Kijiji na Wananchi kwa ujumla.
Akizindua zoezi la upandaji wa Miti katika Shamba la Kijiji cha Mugunzu, siku ya Jumanne tarehe 22.11.2022, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kaimu Katibu Tawala Patrick Kechegwa katika hotuba yake alitoa wito kwa viongozi wote wa Kata na Vijiji kuendelea na kampeni ya upandaji miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti iliyopandwa inakuwa na kutunzwa.
“Viongozi wa Kata na Vijiji simamieni vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vinatuzwa na kulindwa, Wananchi wasitishe shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kwani hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokaidi, Alisema Kechengwa.
Aliongeza kuwa kila kaya ipande na kutunza angalau Miti 10 katika eneo lao, vile vile Taasisi za Serikali, binafsi na Taasisi za dini wapande miti katika maeneo yao”.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la DRC ambalo limefadhili zoezi la upandaji wa miche, Alfred Magehema aliwasisitiza wananchi kuhimizana na kushirikiana kwani suala la utunzaji wa Mazingira ni la watu wote.
Aliongeza kuwa Shirika litaendelea kuwekeza katika Mazingira kwa kushirikiana na Serikali na DRC itapanda Miche laki tatu na elfu ishirini (320,000) kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira. Kwa sasa Shirika la DRC lina vitalu vinne vya Miche ndani ya Wilaya ya Kakonko,
Afisa Maliasili Wilaya ya Kakonko Melkizedek Huruma alieleza kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, Halmashauri inatakiwa kupanda miche milioni moja na laki tano (1,500,000) katika maeneo mbali mbali ya Vijiji.
Ili kutimiza malengo hayo, Afisa Maliasili alieleza kuwa wamekuwa wakishirikisha Taasisi binafsi, Mashirika na wadau wenye ni njema. Aliendelea kusema kwa sasa kuna miche zaidi ya laki tatu (300,000) kutoka kwenye vitalu vilivyofadhiliwa na Shirika la DRC, vile vile watu binafsi wana miche laki mbili (200,000) hivyo mpaka sasa Wilaya ya Kakonko ina jumla ya miche laki tano (500,000).
Mmoja wa Wananchi walioshiriki zoezi la kupanda miche bwana Baraka alipongeza na kuishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa kushirikiana na Shirika la DRC kufanikisha zoezi hilo na kuahidi kuitunza miti hiyo. Aidha aliliomba Shirika la DRC kuendelea kuwapelekea fursa mbalimbali za miradi katika kata ya Mugunzu.
Wananchi wa Kata ya Mugunzu Wilayani Kakonko wameshiriki zoezi la uzinduzi wa upandaji Miti katika eneo la shamba la Kijiji lililopo kata ya Mugunzu. Zoezi hilo limeendeshwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ambaye ni Kaimu katibu tawala Ndugu Patrick Kechegwa kwa kushirikiana na wafadhili ambao ni Shirika la DRC (Danish Refugee Council).
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa